Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilianzishwa tarehe 11 Oktoba, 2024 chini ya Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Na. 08 ya Mwaka 2024. kwa lengo la kuanzisha, kusimamia, kuendesha na kuendeleza viwanja vya ndege vya Serikali Tanzania Bara. Taasisi hii inayo majukumu kadhaa yakiwemo: -
Historia ya usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania Bara inaanzia baada ya uhuru wa Tanganyika hadi miaka ya 1998, ambapo masuala haya yalikuwa yakiratibiwa na Kitengo cha Viwanja vya Ndege kilichokuwa chini ya Wizara zilizokuwa zinahusika na masuala ya Usafirishaji.
Kufuatia mageuzi ya kiuchumi na kimifumo nchini yaliyolenga kuziwezesha Idara na Kurugenzi za Serikali kutekeleza majukumu yao kwa haraka na kuongeza ufanisi, Idara ya Viwanja vya Ndege ilifutwa na kuanzisha Wakala wa Viwanja vya Ndege Tanzania ambayo iliitwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (Tanzania Airports Authority - TAA).
Wakala wa Viwanja vya Ndege Tanzania ulianzishwa tarehe 29 Novemba 1999 kwa Tangazo la Serikali Na. 404 la mwaka 1999. Wakala huo ulipewa jukumu la kutekeleza yaliyokuwa majukumu ya Idara ya Viwanja vya Ndege chini ya Sheria ya Viwanja vya Ndege (Utoaji wa Leseni na Udhibiti) Sura ya 92. Aidha, Tangazo hilo lilielekeza TAA kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria zinazohusu leseni na udhibiti wa Viwanja vya Ndege; Tozo za huduma za Viwanja vya Ndege; udhibiti wa usafiri wa anga; huduma za zimamoto na uokoaji pamoja na kanuni mbalimbali.
Katika kuendelea kuimarisha usimamizi wa viwanja vya ndege, mwezi Oktoba 2024 Serikali ilitunga rasmi Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bara ambayo iliianzisha TAA na kuipa jukumu la kuanzisha, kuendeleza, kusimamia, kuendesha na kutunza viwanja vya ndege vya Serikali Tanzania Bara.