Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania Bw. Abdul Mombokaleo, leo septemba 22, amekabidhi hundi ya kiasi cha shilingi Bilioni 20 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha CPA Mohamed Seif kwa ajili ya malipo ya awamu ya tano kwa wananchi wa Mtaa wa Kipunguni wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Abdul Mombokaleo, amewashukuru wananchi wa Kipunguni kwa uvumilivu wao na kueleza kuwa zoezi la ulipaji wa fidia linaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Serikali hii ni sikivu na inajua umuhimu wa kulipa madeni. Tunafanya malipo kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha na kwa kiwango kinachostahili,” amesema Mombokaleo.
Pamoja na hayo Bw. Mombokaleo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutambua umuhimu wa kulipa fidia kwa wananchi wa Kipunguni na kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuwalipa wananchi hao, ambapo hadi sasa jumla ya wakazi 717 wameshalipwa kiasi cha Tsh Bilioni 66 kati ya wananchi 1,864 waliofanyiwa tathmini ambao wanatakiwa kulipwa kiasi cha Tsh Bilioni 144.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Fedha CPA Mohamed Seif amesema malipo hayo yataanza kulipwa rasmi tarahe 28 septemba, 2026 kwa awamu ambapo wananchi watakaotakiwa kulipwa kwa awamu hii watajulishwa kupitia ofisi ya serikali ya mtaa wa Kipunguni.