Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MSALATO WA FIKIA 94%


image title here


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo, amesema kuwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), umefikia hatua kubwa ya ukamilishaji.

“Hadi sasa, kazi za miundombinu zimefikia asilimia 94% na ujenzi wa majengo upo katika hatua ya asilimia 60%. Hii ni hatua ya kujivunia kwani tunaona ndoto ya Serikali ya Awamu ya Sita ikitimia ya kujenga kiwanja cha kisasa kitakachokuwa kitovu cha biashara, utalii na usafirishaji wa bidhaa za kilimo na viwandani kwenda masoko ya kimataifa,” alisema Bw. Mombokaleo.

Mradi huu unajumuisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege ya daraja 4E, yenye uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za abiria na mizigo, barabara za viungio, maegesho ya ndege, mfumo wa taa za kuongozea ndege, pamoja na jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka. Aidha, unahusisha ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege, kituo cha zimamoto, maegesho ya magari, barabara za kuingilia kiwanjani na uzio wa usalama.

Mradi unatekelezwa kwa awamu mbili (Lot 1 na Lot 2) ambapo Lot 1 umegharimu Shilingi Bilioni 165 na Lot 2 Shilingi Bilioni 194.

“Huu si mradi wa kiwanja cha ndege pekee, bali ni mradi wa kimkakati wa taifa. Ni injini ya uchumi itakayosukuma mbele biashara, uwekezaji na kukuza utalii, sambamba na kuitangaza Tanzania kimataifa. Tunatoa shukrani zetu kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa dhamira na uwekezaji mkubwa katika sekta ya anga,” aliongeza Bw. Mombokaleo.

Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kinatarajiwa kuwa lango kuu la kuingia Makao Makuu ya Nchi – Dodoma, na kuchochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa taifa.