Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imepokea Tuzo mbili kupitia viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere na Kilimanjaro kwa ajili ya ubunifu na maendeleo endelevu kwa mazingira Katika viwanja hivyo vya ndege pamoja na kutambua hatua thabiti zilizochukuliwa katika kupunguza athari za mazingira ikiwa ni sehemu ya mwitikio wa kimataifa wa sekta ya usafiri wa anga upande wa viwanja vya ndege dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Tuzo hizo zilizotolewa na Baraza la Viwanja vya ndege Afrika (ACI) zimekabidhiwa kwa TAA na Rais wa Baraza hilo Bw. Emanuel Chaves pamoja Katibu Mkuu Bw. Ali Tounsi, katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Ciela Resort, Jijini Lusaka, Zambia.
Akipokea tuzo hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato, Bw. Clemence Jingu, amesema kuwa hatua hiyo ni mwanzo muhimu kwa Mamlaka katika kutekeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Bw. Jingu ameeleza kuwa TAA tayari imefanya utambuzi wa vyanzo mbalimbali vya uchafuzi wa mazingira na sasa inaandaa mikakati madhubuti ya kupunguza athari hizo, sambamba na Agenda ya Net Zero ifikapo mwaka 2050.
Aidha, Bw. Jingu amesisitiza kuwa TAA itaendelea kushirikiana na wadau wake, hususani mashirika ya ndege, ili kuhakikisha kuna mtazamo wa pamoja katika juhudi za kulinda mazingira.
Hata hivyo alibainisha kuwa mpango huu utaendelezwa katika viwanja vingine vya ndege nchini.
Ikumbukwe kuwa dunia kwa sasa ipo katika jitihada kubwa za pamoja za kulinda mazingira na ustawi wa vizazi vijavyo, ambapo sekta ya usafiri wa anga ina nafasi kubwa ya kuonesha mfano wa utekelezaji endelevu wa mikakati ya kupunguza hewa ukaa.
Mkutano Mkuu wa 34, Mkutano wa Bodi, Kikanda na Maonesho umefunguliwa rasmi leo tarehe 18 Septemba, 2025 baada ya kutanguliwa na Vikao vya kamati mbalimbali zilizojadili masuala ya Rasilimali watu, Mazingira, Teknolojia, uwezeshaji, Usalama na Ufundi ili kuongeza ubunifu na ukuzaji maarifa katika nyanja hizo katika Viwanja vya ndege Barani Afrika.