Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

TAA NA TRC WATIA SAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO USAFIRI WA ANGA NA RELI NCHINI.


image title here


Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) leo wametia saini hati ya makubaliano ya kuunganisha usafiri wa anga na reli nchini, hatua inayolenga kuimarisha huduma kwa abiria na wasafirishaji wa mizigo kwa kuunganisha miundombinu ya viwanja vya ndege na reli. Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Abdul Mombokaleo, na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mha. Machibya M. Shiwa.

Akizungumza mara baada ya kutia saini hati ya makubaliano hayo, Mha. Machibya amesema ushirikiano huo utawezesha wasafiri kuingia na kutoka katika viwanja vya ndege kwa urahisi zaidi kupitia huduma za reli, amebainisha kuwa hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt, Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa Bandari ya Kwala, ambapo aliagiza TRC kufungua vituo vyenye miundombinu itakayowezesha kuunganisha reli na viwanja vya ndege. “Kwa sasa upembuzi yakinifu katika Kiwanja cha Ndege cha JNIA umekamilika, na kwa Kiwanja cha Ndege cha Msalato mchakato unaendelea, pia katika Kiwanja cha Ndege cha KIA, tayari kuna miundombinu ya reli ya MGR ambayo itakarabatiwa na kujengwa kituo cha treni amesema”. Vile vile Mha. Machibya ameendelea kusema kuwa maboresho haya yatawezesha kukuza shughuli za utalii, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika kwa haraka (perishable goods), na kupunguza gharama kwa wasafiri na wasafirishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Abdul Mombokaleo amesema ushirikiano huu ni hatua muhimu kwa maendeleo ya taifa kwani utaimarisha sekta ya anga na reli kwa pamoja. Mashirikiano haya yatachangia kukuza uchumi wa nchi, kuongeza pato la taifa na kuboresha sekta ya usafiri wa anga na reli na kuimarisha ongezeko la abiria na mizigo, Pia yatasaidia kuimarisha urahisi wa usafirishaji wa mizigo inayosafirishwa nje ya nchi (export cargo)
Aidha, ameongeza kuwa huduma za kisasa kama remote check-in na drop-off zitatolewa nje ya viwanja vya ndege ambapo zitawezesha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka kwenye vituo vya treni kwenda viwanja vya ndege.