Shirika la ndege la Neos Air kutoka Italia leo limezindua rasmi huduma ya safari za moja katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), kufuatia kuwasili kwa ndege yake kwa mara ya kwanza katika kiwanja hicho. Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa muunganiko wa usafiri wa anga kati ya Tanzania na Ulaya.
Uzinduzi wa safari hiyo uliambatana na hafla fupi ya ukaribisho iliyoandaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kushirikiana na Neos Air katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro, ikihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta za usafiri wa anga na utalii.
Kupitia safari hiyo mpya, Neos Air itakuwa ikifanya safari zake mara moja kwa wiki kila Jumatano, zikianzia Milan Malpensa nchini Italia kuelekea Kilimanjaro, kisha Zanzibar, kabla ya kurejea Milan, ikitumia ndege yake aina ya Boeing 787-9.
Kuanzishwa kwa safari hizo kunalenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kitalii kati ya Tanzania na Italia, pamoja na kuongeza fursa kwa watalii kusafiri moja kwa moja kuelekea Kaskazini mwa Tanzania kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro