Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imelipa jumla ya shilingi bilioni 20 kama fidia wananchi wa Mtaa wa Kipunguni, Jimbo la Segerea, Dar es Salaam ambao wamepisha upanuzi wa Kiwanja chachacha Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ulipaji wa fidia, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, amesema serikali imetenga fedha kwa awamu ya kwanza ili kuwalipa waliostahili. Amesisitiza kuwa malipo haya ni haki ya wananchi na yanafanyika kwa maslahi mapana ya taifa.
Mombokaleo ameongeza kuwa zoezi hili la ulipaji fidia ni endelevu na halihusishi Dar es Salaam pekee, bali litaendelea katika mikoa mingine nchini. Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ina mpango wa kuhakikisha watu wote wanaodai fidia wanalipwa hadi pale zoezi litakapokamilika.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bertha Bankwa, amewashukuru wananchi kwa kushirikiana na serikali kwa kupisha upanuzi wa uwanja huo. Amesema maboresho hayo yatawezesha kiwanja kupanda daraja kutoka 4C hadi 4F, hatua itakayoruhusu ndege kubwa kutua bila changamoto yoyote.
Bertha ameongeza kuwa upanuzi huo utatoa fursa mbalimbali za uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa mahoteli, kumbi za mikutano na karakana, ambazo zitachangia kuongeza pato la kiwanja na kuimarisha ulinzi wa uwanja huo. Pia, hatua hiyo itasaidia kupunguza athari za kelele kwa wakazi wa maeneo jirani.
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kwa niaba ya wananchi, ametoa shukrani kwa serikali na timu nzima ya TAA kwa kufanikisha ulipaji huo wa fidia. Amesema malipo hayo yameleta matumaini kwa wananchi wa Kipunguni waliokuwa wakidai fidia kwa muda mrefu.