Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

SEHEMU YA BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI KWA MWAKA 2025/2026 KATIKA VIWANJA VYA NDEGE


image title here


Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeendelea kusimamia, kuendesha na kuendeleza Viwanja 61 vya Ndege vya Serikali Tanzania bara. Hadi kufikia Machi 2025, Serikali kupitia TAA imeendelea na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambapo ujenzi wa jengo jipya la abiria umekamilika, na kazi ya ufungaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege (AGL) inaendelea.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, kazi ya ukamilishaji wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza imefikia asilimia 13; kazi ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi imefikia asilimia 69; na Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali wa kiwanja kipya cha Ndege cha Njombe umekamilika na taratibu za utwaaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi zinaendelea. Vilevile, Wakandarasi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Lindi na mradi wa ujenzi wa jengo la abiria, jengo la mnara wa kuongozea ndege, kituo cha hali ya hewa na kituo cha zimamoto katika Kiwanja cha Ndege cha Mtwara wamekabidhiwa maeneo ya mradi na taratibu za malipo ya awali zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa ndege zinazotumia Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Serikali imeona umuhimu wa kujenga mnara wa kuongozea ndege katika Kiwanja hicho ambapo maandalizi ya awali yanaendelea. Aidha, Serikali inaendelea na mpango wa kudumu wa kutatua changamoto za usalama katika usafiri wa anga katika Mkoa wa Kagera. Katika utekelezaji wa Mpango huo, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imependekeza eneo jipya litakalofaa kwa ujenzi wa Kiwanja kipya cha Ndege cha Daraja la 4C ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege zinazobeba abiria hadi 220 kwa wakati mmoja. Pendekezo hilo lilionesha eneo la Kyabajwa lililopo Wilaya ya Misenyi kufaa zaidi kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja kipya. Kwa sasa taratibu za utwaaji ardhi zinaendelea.