Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

Naibu Waziri wa Uchukuzi David kihenzile afanya ziara katika kiwanja cha ndege cha Arusha


image title here


Naibu Waziri wa Uchukuzi David kihenzile amesema kukamilika kwa jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Arusha kutawezesha abiria takribani laki nne kuhudumiwa kupitia Kiwanja hicho kwa mwaka.

Kihenzile ameyasema hayo baada ya kukagua maendeeleo ya mradi wa jengo la abiria katika kiwanjani hapo ambao kwa sasa umefikia asilimia 98 na kusema kukamilika kwa jengo hili kutarahisisha utoaji wa Huduma kwa abiria wanaowasili na kuondoka kiwanjani hapo.

“Kukamilika kwa jengo hili kutatua changamoto ya utoaji wa Huduma kwa abiria wanaowasili na kuondoka sababu jengo la kwanza lilikuwa dogo sana , hatuna budi kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuruhusu Uwekezaji huu mkubwa katika usafiri wa anga” amesema Naibu Waziri Kihenzile.

Naibu Waziri Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kumsimamia Mkandarasi Zhixin Construction Limited na kuhakikisha jengo Hilo linakamilika kwa viwango vilivyokubalika kwenye Mkataba.

Aidha, Naibu Waziri Kihenzile ametanabaisha kuwa tayari Serikali kupitia TAA imeshaanza kutekeleza mradi wa kuweka taa za kuongozea Ndege ili kukiwezesha Kiwanja hicho kutoa huduma kwa saa 24.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Arusha Godfrey Kaaya amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa kazi ndogo ndogo zilizobaki za jengo hili zitakamilika ndani ya wiki moja na hivyo kuweza kutoa huduma kwa abiria wanaowasili na kuondoka.

Meneja Kaaya ameongeza kuwa katika kuendelea kuboresha huduma na kuongeza mapato Serikali inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa Hotel yenye hadhi ya Nyota nne katika kiwanja cha ndege Arusha Mradi utakaotekelezwa kwa ubia kati kushirikisha sekta binafsi.