Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

NAIBU WAZIRI UCHUKUZI ARIDHISHWA NA KASI UJENZI UWANJA WA NDEGE MSALATO.


image title here



Naibu waziri wizara ya Uchukuzi David Kihenzile ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma ambao umefikia asilimia 67.6 kwa upande wa miundombinu ya njia ya kurukia ndege huku ukiwa umefikia asilimia 32.21 kwa upande wa jengo la abiria.
Naibu Waziri Kihenzile amesema ameridhishwa kwa kujengwa kwa njia ya kurukia ndege yenye urefu wa Kilometa 3 na mita 600 pamoja na eneo litakalokuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa 13 kwa wakati mmoja lenye urefu wa mita 480.
“Nimeshuhudia maendeleo mazuri ya ujenzi wa jengo la zima moto, Jengo la hali ya hewa pamoja na mnara wa kuongozea ndege kimsingi uwanja huu utakapokamilika utakuwa wenye tija kubwa hususani katika Nyanja ya utalii,” Ameongeza Naibu Waziri kihenzile.
Aidha Naibu Waziri Kihenzile ameupongeza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kuendelea kufanya kazi nzuri katika kusimamia ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025.
Ujenzi wa kiwanja cha ndege Msalato unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 165.6 kwa mradi wa njia ya kutua na kuruka ndege huku ujenzi wa jengo la abiria ukigharimu kiasi cha shilingi bilioni 194.4 na miradi yote ikitarajiwa kukamilika ndani ya miaka 3 kuanzia 2022 hadi mwaka 2025 ambapo mpaka sasa jumla ya wananchi 608 wamepata ajira katika mradi wa ujenzi wa njia ya kutua na kurukia ndege, na wananchi 947 wakipata ajira katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria huku wageni walioajiriwa ni 31 kwa kila mradi. Kiwanja cha ndege Msalato kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.