Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

MKURUGENZI MKUU TAA AKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI KATIKA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA KILIMANJARO.


image title here


Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo, leo amefanya ziara ya kikazi katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Abiria la Watu Mashuhuri (Uhuru VIP Terminal), jengo la Jeshi la Zimamoto uokoaji,jengo la mgahawa wa wafanyakazi,pamoja na kufanya kikao kazi na Menejimenti ya kiwanja hicho ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.

Katika ziara hiyo, Bw. Mombokaleo alipokea taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Jengo la Abiria wa watu Mashuhuri (Uhuru VIP Terminal), ambalo linatarajiwa kuongeza hadhi ya KIA kwa kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni, viongozi wa kitaifa na kimataifa pamoja na wawekezaji, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya utoaji wa huduma za viwanja vya ndege.

Aidha, amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Jeshi la Zimamoto na uokoaji pamoja na jengo la mgahawa wa wafanyakazi, miradi inayolenga kuimarisha mazingira ya kazi, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuboresha miundombinu ya kiutendaji katika kiwanja hicho.

Akikagua maeneo ya miradi hiyo, Mkurugenzi Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zinatekelezwa kwa kuzingatia ubora, usalama, thamani ya fedha na muda uliopangwa, ili miundombinu hiyo ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wakati, sambamba na kukidhi matarajio ya wadau wa sekta ya usafiri wa anga.

Aidha, katika kikao chake na Menejimenti ya KIA, wamejadili masuala ya uendeshaji wa kiwanja, ikiwemo kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha usalama wa viwanja vya ndege, kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku pamoja na maandalizi ya utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo inayolenga kuongeza uwezo wa kiwanja hicho kuhudumia ongezeko la abiria na ndege.

Bw. Mombokaleo ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa TAA wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya viwanja vya ndege ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga na kuchochea sekta ya utalii.