Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndge Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo, amefanya ziara ya kikazi katika Kiwanja cha Ndege Arusha kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi wa usimikaji wa taa za kuongozea ndege (Airfield Ground Lighting – AGL), mradi unaotarajiwa kubadili historia ya uendeshaji wa kiwanja hicho kwa kuruhusu ndege kutua na kuruka wakati wa mchana na usiku kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
Akiwa katika ukaguzi huo, Bw. Mombokaleo ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati huku viwango vya ubora na usalama vikizingatiwa ili wananchi na wadau wa sekta ya usafiri wa anga waanze kunufaika na huduma hiyo kama ilivyopangwa.
Amesema kukamilika kwa mradi huo ni hatua kubwa katika jitihada za Serikali kupitia TAA za kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege, kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta za utalii, biashara na uwekezaji.
"Kuanzishwa kwa huduma za ndege usiku na mchana katika Kiwanja cha Ndege Arusha kutapanua uwezo wa kiwanja hiki kuhudumia safari nyingi zaidi, kuongeza usalama wa safari na kuwapa wawekezaji na watalii urahisi mkubwa wa kufika katika vivutio vya utalii vilivyopo Kaskazini mwa Tanzania," amesema Bw. Mombokaleo.
Kiwanja cha Ndege Arusha ni miongoni mwa viwanja vya ndege muhimu vinavyohudumia sekta ya utalii nchini, kikiwa lango kuu la wasafiri wanaoelekea katika Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Ziwa Manyara pamoja na Mlima Kilimanjaro. Maboresho yanayoendelea yanatarajiwa kuongeza ushindani wa sekta ya anga na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.
Aidha, maboresho hayo yanakuja wakati Mkoa wa Arusha ukiendelea kujiandaa kupokea matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo mashindano ya AFCON na Miss World, yanayotarajiwa kuongeza idadi ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi.