Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2005; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

KAMATI YATAKA MAENEO YA VIWANJA VYA NDGE YAWE NA HATIMILIKI


image title here


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa hatimiliki za maeneo ya Viwanja vya Ndege vyote nchini ili kudhibiti uvamizi katika maeneo hayo na kupelekea ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi.

Agizo hilo limetolewa Machi 14, 2024  Mkoani Shinyanga na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso (Mb) wakati walipokuwa wakikagua ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga ambao utekelezaji wake kwa sasa umefikia asilimia 10.4.

“Hakikisheni mnasimamia maeneo yenu kwa kupata haki miliki katika Viwanja vya Ndege vyote pamoja na kuweka mawe ya alama maeneo ambapo viwanja vinaishia ili kuzuia wananchi wanaoingia kwenye maeneo yenu kiholela”, amesisitiza Kakoso.

Kamati imeitaka Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wananchi wananufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini kwa kupewa huduma mbalimbali zinazoigusa jamii ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati na visima vya maji.

Aidha, Kamati imempongeza  Waziri wa Ujenzi kwa kuendelea  kufuatilia kwa ukaribu upatikanaji wa fedha katika miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikichelewa kukamilika kutokana na malipo kutolipwa kwa wakati.
Kamati pia imepongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha na kukarabati viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga, Sumbawanga na Kigoma ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameihakikishia Kamati kuwa timu ya TANROADS imejipanga kumsimia kikamilifu Mkandarasi kukamiliisha ujenzi wa Kiwanja hicho ifikapo mwezi Oktoba, 2024.

“Niwahakikishie  tumejipanga kumsimamia Mkandarasii kwani asilimia 80 ya vifaa tayari vipo site, hadi kufikia Julai 30 barabara ya kuruka na kutua ndege itakuwa tayari inaaza kutumika katika Kiwanja hiki na huku kazi zingine zikiendelea”, amefafanua Bashungwa.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga, ameeleza kuwa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, ofisi mbalimbali, sehemu za biashara, ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (Km 2.2), barabara ya unganishi, ujenzi wa eneo la kuegesha magari, ujenzi na ufungaji wa mnara wa kuongoza ndege, ujenzi wa mifereji ya maji, usimikaji wa mifumo ya taa za kuongozea ndege na ujenzi wa uzio wa usalama.