Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

JNIA NA KIA ZANG’ARA TUZO ZA ACI AFRICA NIGERIA.


image title here


Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) vimeipa Tanzania heshima kubwa barani Afrika baada ya kutwaa tuzo tatu zilizotolewa na Baraza la Viwanja vya ndege Afrika (ACI Africa), jijini Abuja, Nigeria.

Katika tuzo hizo, JNIA imefanikiwa kupata tuzo mbili, ikiwamo nafasi ya pili katika katika kipengele cha Utawala Bora upande wa uwezeshaji na utayari wa huduma za abiria (Runner-Up of Passenger Facilitation and Readiness Excellence Awards 2026 in the Governance category) na nafasi ya pili katika kipengele cha Ubunifu na Mageuzi ya kiteknolojia (Innovation & Transformation category), katika kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia abiria kati ya milioni 2 na milioni 5 kwa mwaka.

KIA imeibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa Uwezeshaji na Utayari wa Huduma kwa Abiria 2026 katika kipengele cha Ushirikishwaji wa Wadau, kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia abiria chini ya milioni 2 kwa mwaka.

Tuzo hizo zimepokelewa na Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo Bw. Mzee Kilele kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo, katika hafla iliyofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 35 wa ACI Africa, unaoendelea jijini Abuja ulioanza tarehe 19 na kufungwa tarehe 25 Septemba 2026. Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo “Next-Gen Airports: Driving Performance and Resilience”, unaolenga kujadili namna ya kuimarisha utendaji, ubunifu, teknolojia na ustahimilivu wa viwanja vya ndege barani Afrika.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo ,Mkurugenzi wa Biashara, Bw. Mzee Kilele, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa juhudi zinazofanywa na TAA katika kuboresha huduma, kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na kuweka mazingira bora ya kukuza shughuli za kibiashara na kiundeshaji katika viwanja vya ndege nchini.

Tuzo hizi ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na TAA kwa kushirikiana na wadau pamoja na ukuaji wa viwanja vya ndege unaoenda sambamba na ubora wa huduma, ubunifu na uwezo wa kujenga mahusiano imara na wadau katika sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.