Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

ARUSHA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA 73 WA BARAZA LA VIWANJA VYA NDEGE AFRICA


image title here


ARUSHA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA 73 WA BARAZA LA VIWANJA VYA NDEGE AFRICA

Mkoa wa Arusha utakuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa 73 wa Kikanda wa Baraza  la viwanja vya ndege  Afrika na maonesho ya wadau utakaowakutanisha Wataalamu mbalimbali kutoka kwenye mashirika ya ndege, Makampuni na taasisi za Kimataifa za usafiri wa anga zaidi ya 400, ukitarajiwa kufanyika kwa siku saba kuanzia Aprili 24- 30, 2025.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kiwanja  cha  ndege Arusha wakati akizungumza na wanahabari leo Januari 08, 2025, amesema maandalizi ya mkutano huo yanakwenda vizuri, akiushukuru Uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mhe. Paul Christian Makonda kwa ushirikiano wao, huku akiwasihi wakazi wa Arusha kutumia ujio wa wajumbe wa mkutano huo kujipatia kipato na kujinufaisha Kiuchumi.

Kwa upande wake Mhe. Paul Christian Makonda aliyeambatana na Mhe. Mbarawa, ameshukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wizara hiyo kwa Kuiteua Arusha kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, akiahidi usalama wa kutosha pamoja na huduma nzuri kwenye maeneo ya malazi na kumbi za mikutano kwa wageni wote kwa siku zote saba za kufanyika Mkutano huo.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Waziri Mbarawa, Wajumbe hao zaidi ya mia nne, kwenye siku zao saba za kuwa Mkoani Arusha wametenga siku moja kwaajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya Utalii Mkoani Arusha suala ambalo linatajwa na Mhe. Makonda kwamba litakuwa sehemu nyingine ya kusisimua uchumi wa Mkoa wa Arusha kupitia sekta ya Utalii na sekta nyingine mtambuka za vyakula, usafiri, sehemu za starehe, hoteli na nyumba za kulala wageni.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Abdul Mombokaleo  amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini ni fursa kwa nchi kujitangaza na kuwezesha ushirikishwaji wa wadau katika mkutano huu  huku akielezea hatua za awali za maandalizi ya mkutano huo ikiwemo mkakati wa utafutaji wa fedha.