Kiwanja cha Ndege Songwe
Historia fupi ya Kiwanja
Kiwanja cha ndege cha Songwe ni moja kati ya viwanja 59 vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kiwanja hiki kilianza shughuli za uendeshaji mwaka 2012 baada ya kufungwa kwa kiwanja cha zamani cha ndege kilichopo Mbeya mjini na kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu muhimu ya kiwanja hiki cha Songwe ikiwemo Jengo la abiria, Jengo la kuongozea ndege, Jengo la zimamoto, kituo cha utabiri wa hali ya hewa, barabara ya kutua na kurukia ndege, maegesho ya ndege, barabara ya kiungio na maegesho ya magari. Hapo kabla, huduma za ndege zilikuwa zikifanyika kiwanja cha Mbeya mjini pale eneo la Mwanjelwa.
Kwa sasa kiwanja kina uwezo wa kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200. Kiwanja kipo daraja 4C, ICAO Code HTGW, IATA code MBI. Zimamoto ni Daraja la 6.
Viwanja vidogo vya Chunya na Mbeya
Kiwanja cha ndege cha Songwe pia kinasimamia viwanja vidogo vilivyoko Mkoani Mbeya ambavyo viko chini ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania.
Kiwanja cha ndege Chunya.
Kiwanja hiki kilianzishwa enzi za Ukoloni miaka ya 1939 kikilenga kuhudumia ndege za walowezi wa mashamba ya Tumbaku na uchimbaji wa madini. Kiwanja hiki kina urefu wa mita 1,200 na upana wa mita 30. Kimejengwa kwa kiwango cha nyasi. Kina eneo lenye ukubwa wa Mita za mraba 636,658.
Kiwanja kidogo cha Ndege Mbeya
Kiwanja hiki pia ni kati ya viwanja vya zamani ambapo kwa sasa kimefungwa na eneo lake limebadilishiwa matumizi baada ya shughuli za usafiri wa anga kuhamishiwa Kiwanja cha ndege Songwe tarehe 13 Disemba 2012.
Miundombinu ya kiwanja
Kiwanja cha ndege Songwe kina barabara ya kutua na kurukia Ndege yenye uelekeo 09/27 yenye urefu wa Mita 3330 na upana wa Mita 45(Lami yenye PCN 57) njia ya kuingilia kiwanjani( Taxway) yenye upana wa Mita 23 . Eneo la maegesho ya ndege (Apron) lina urefu wa Mita 194.66 na upana wa Mita 89.6 sawa na Mita za mraba 17,400.54 linaweza kuegesha Ndege 5 za Daraja C (mfano bombardier Q 400) kwa wakati mmoja.
Miundombinu na vifaa kwenye eneo la Kiwanja.
Kiwanja kina jengo la kuongpozea Ndege (control Tower), Rada, GNSS, na NDB, Taa za kuongozea Ndege (PAPI, AGL), Kituo cha hali ya hewa (OBS)
Maegesho ya magari yenye jumla ya eneo la Mita za Mraba 10274.66 na linaweza kubeba magari 400 kwa wakati mmoja. Pia kuna huduma za msingi kama vile ATM mashine ya benki ya CRDB ( inapokea VISA, Masta kadi nk) Mgahawa, Ofisi za mashirika ya ndege na Jengo la utawala.
Huduma ya Zimamoto na Uokoaji
Kituo cha Zimamoto kipo kwenye daraja 6 kwa mujibu wa viwango vya ICAO. Kina magari mawili (02) pamoja na mitambo mingine ya kuzimia moto.
Udhibiti wa ndege hai na Wanyama
Katika kuhakikisha usalama wa kiwanja unakuwepo wakati wote, kipo kitengo mahususi cha kukabiliana na Wanyama na ndege hai. wanaoishi kuzunguka eneo la Kiwanja.
Mashirika ya ndege yanayotoa huduma
Kiwanja kinatoa huduma kwa ndege zenye ratiba maalumu na zile zisizokuwa na ratiba maalumu (Adhoc). Hivi sasa tuna mashirika ya ndege ya ATCL na Precision Air yenye ratiba maalumu.
Wateja wa pango
Miradi inayotekelezwa na TAA
katika mwaka huu wa fedha, Kiwanja cha Ndege cha Songwe kinaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ni pamoja na kufanya matengenezo ya Jengo la Utawala, ukarabati wa mfumo wa umeme kutoka katika Jengo la jenereta, usimikaji wa UPS kwa ajili ya taa za AGL, Ununuzi wa vifaa kinga vya Zimamoto na ununuzi wa vifaa vya mawasiliano. Miradi yote hii ipo katika hatua mbalimbali za Ununuzi.