Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Kiwanja Cha Ndege


Picha za Viwanja Vya Ndege
Taarifa za Viwanja vya Ndege

Kiwanja cha Ndege Mwanza

Historia fupi ya Kiwanja.

Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ni miongoni mwa viwanja vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, kikiwa kiwanja cha tatu kwa ukubwa kikitanguliwa na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam (JNIA) na Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA). Kiwanja hiki kiko kwenye Daraja la ukubwa 4C kikiwa na daraja la saba la Viwango vya Zimamoto na Uokoaji (Fire Cat 7).

Historia ya kiwanja cha ndege cha Mwanza ilianzia miaka ya 1940 ambapo kilikuwa kinamilikiwa na Williamson Diamonds ambaye alikuwa anakitumia kusafirisha madini aina ya Almasi kutoka Mwadui kwenda Nairobi nchini Kenya. Awali kiwanja hiki kilikuwa kwenye eneo la Butuja (Viwanja vya Sabasaba) lakini kutokana na eneo hilo kukatisha barabara ya magari na kuhatarisha usalama wa watu na ndege, mwaka 1958 kiwanja hicho kilihamishiwa katika kijiji cha Kisaka(mahali kilipo hivi sasa). baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 Disemba kiwanja kilichukuliwa na Serikali ambapo kuanzia miaka ya 1970 Serikali ilianza kufanya maboresho mbalimbali ya kukifanya kiwanja kutoka kiwanja kidogo na kuwa kiwanja kikubwa.

MIUNDO MBINU YA KIWANJA

Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kina Miundo mbinu mbalimbali ikiwemo barabara kuu ya kurukia ndege (Runway) yenye urefu wa Kilometer 3.8 na upana wa mita 45 kukiwa na maegesho matatu (3) ya ndege na viunganishi (Taxiways) saba (7), Jengo moja la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja, Ukumbi wa watu mashuhuli (VIP), Kituo cha Zimamoto chenye Magari matatu (3) ya zimamoto na uokoaji yenye uwezo wa kubeba lita 26,000 za maji na madawa ya kuzimia moto lita 2,600, Majenereta manne (4), Mifumo ya usalama (CCTV), Mifumo ya Maji safi na taka, Maegesho ya Magari na Jengo la kuongozea Ndege (Control tower). baadhi ya miundo mbinu iliyoelezwa ni matokeo ya upanuzi na maboresho ya Kiwanja uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano hususani kwenye maeneo yafuatayo;

Urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa mita mia tano (500m) na upana wa mita arobaini na tano (45) na kufanya barabara ya kutua na kuruka ndege kuwa yenye urefu wa kilomita 3.8 ambayo ni ndefu kuliko viwanja vyote Tanzania;

Ujenzi wa jengo la kisasa la kuongezea ndege (control tower);

Ujenzi wa maegesho ya kisasa ya ndege za abiria na mizigo;

Uchepushaji wa mto;

Ujenzi wa jengo la kisasa la mizigo lenye eneo la mita za mraba 541

Usimikaji wa mifumo ya maji safi na taka;

Ujenzi wa kituo cha kufua umeme chenye majenereta mawili yenye uwezo wa kuzalisha umeme kVA 650 kila moja;

Usimikaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege (AGL);

Na hivi karibuni Serikali imesimika mtambo wa kuongozea ndege (radar).

Matokeo ya Uendelezaji wa Miundo mbinu ya Kiwanja

matokeo ya maboresho ya miundo mbinu tajwa hapo juu yameleta ufanisi mkubwa kwenye shughuli za uendeshaji hapa kiwanjani kama ifuatavyo;

Urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege umewezesha ndege kubwa kama B787 Dream liner kutua katika kiwanja chetu;

Ujenzi wa maegesho ya Ndege umeongeza uwezo wa Kiwanja kuhudumia Ndege nyingi kwa wakati mmoja;

Uchepushaji wa mto umeweza kutatua changamoto ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea na kuzuia kuzuia shughuli za uendeshaji;

Ujenzi wa jengo la kisasa la mizigo umewezesha kiwanja kuhudumia mizigo ya aina zote ikiwa ni pamoja ni ile inayoharibika kwa muda mfupi (perishable goods);

Usimikaji wa mifumo ya maji safi na ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 800,000 umetatua changamoto ya upatikanaji wa maji kiwanjani;