Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Kiwanja Cha Ndege


Picha za Viwanja Vya Ndege
Taarifa za Viwanja vya Ndege

Kiwanja cha Ndege Dodoma

UTANGULIZI

Kiwanja cha ndege cha Dodoma ni kati ya Viwanja 59 ambavyo vinasimamiwa, kuendeshwa na kuendelezwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kutokana na viwango vya ICAO, Kiwanja cha Ndege cha Dodoma kipo kwenye daraja la 3C (Code 3C) na daraja la tano la Uzimaji Moto na Uokoaji (Fire Category- CAT 5). Pia, Kiwanja hiki ni miongoni mwa viwanja vinavyotoa huduma kwa Ndege zinazoingia na kutoka nje ya nchi (entry and exit airport).

Kiwanja cha Ndege cha Dodoma kinasimamia pia viwanja vidogo (airstrips) vilivyopo ndani ya Mkoa wa Dodoma (Kondoa, Mpwapwa, Kongwa, Mvumi) na Viwanja vya Mkoa wa Singida (Singida, Kirondatal na Manyoni).

Kiwanja cha Ndege cha Dodoma kilijengwa mnamo mwaka 1945 na utawala wa kikoloni baada ya vita kuu ya pili ya Dunia. Ujenzi huu ulisimamiwa na idara ya kazi (PWD) na ulikuwa katika kiwango cha nyasi lengo likiwa ni matumizi ya usafiri wa haraka wa abiria na mizigo pamoja na kutoa huduma za kijamii kama madawa ya binadamu na wanyama.

Baada ya tamko la Serikali la kuanzisha Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma, kuanzia mwaka 1974 hadi 1976, msukumo wa kuendeleza kiwanja hiki uliongezeka kwa kujenga upya barabara ya kuruka/kutua ndege, viungio vyake na eneo la maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami. Aidha, kuanzia mwaka 2016 hadi 2020, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa njia ya kutua na kuruka ndege (Runway) kutoka meta 2000 hadi meta 2750, maboresho ya maegesho ya ndege (Apron) na barabara za viungio (taxiway), kuweka mfumo wa taa za kuongozea ndege na ujenzi wa sehemu ya kutua helikopta (Helipad).

MIUNDOMBINU YA KIWANJA CHA DODOMA

NJIA YA KURUKA NA KUTUA NDEGE, MAEGESHO YA NDEGE NA BARABARA ZA VIUNGIO

Kiwanja cha Dodoma kina barabara ya kuruka na kutua Ndege (Runway) yenye urefu wa meta 2750 na upana wa meta 30 ambayo imesimikwa Taa za kuongozea ndege (AGL System) zinazotumia mfumo wa jua (solar power); kuna barabara za viungio (Taxiway) tatu (3) na maegesho ya ndege (Apron) yenye uwezo wa kuegesha ndege tatu za Daraja la 3C mfano Bombardier Dash 8 - Q400 na ndege moja ya Daraja la 4C mfano Airbus 220-300 kwa wakati mmoja) na pia kuna kituo cha kutoa huduma ya mafuta ya ndege (PUMA Energy).

JENGO LA ABIRIA NA MIUNDOMBINU YAKE

Kiwanja hiki kina Jengo la abiria lenye ukubwa wa meta za mraba 980 likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 300 (wanaoondoka na wanaowasili) kwa mchanganuo ufuatao; Abiria wanaoondoka – 148, Abiria wanaowasili – 127 na VIP – 25. Aidha, Kiwanja kinatumia umeme wa TANESCO na kina jenereta mbili (Standby Generators - 100Kva na 50Kva).

TAKWIMU ZA NDEGE

Kiwanja cha Dodoma kinahudumia mashirika makubwa mawili ya ndege yenye ratiba maalumu (scheduled flights) ambayo ni Air Tanzania na Precision air. Air Tanzania ina safari 38 kwa wiki na Precision air ina safari 22 kwa wiki. Baadhi ya ndege zingine zinazotua Kiwanjani bila ratiba maalumu (Charter operators) ni pamoja na Tanapa, Air excel, Grumeti, JWTZ, Coastal, Police, Jambo Aviation, TGFA, n.k.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, takwimu za idadi ya safari za ndege inaonesha ongezeko la asilimia 84 kutoka safari za ndege 1,890 mwaka 2016 hadi kufikia safari za ndege 3,475 mwaka 2020. Pia, idadi ya abiria imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 500 kutoka abiria 12,410 mwaka 2016 hadi kufikia abiria 86,056 mwaka 2020. Kuimarika kwa takwimu katika Kiwanja cha Dodoma kumechangiwa zaidi na maamuzi ya Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Kiwanja hiki yanayowezesha Ndege kubwa (mfano Airbus 220-300) kuweza kutua. Michoro hapa chini inafafanua zaidi.

MIRADI YA MAENDELEO ILIYOKAMILIKA, INAYOENDELEA NA INAYOTARAJIWA KUTEKELEZWA

Katika kuhakikisha Kiwanja kinaboresha huduma kwa wadau wake, Serikali imeweza kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo. Miradi iliyotekelezwa na kukamilika katika mwaka 2020/2021 ni pamoja na Mradi wa kurefusha barabara ya kutua na kuruka ndege kwa meta 250 na Mradi wa Upanuzi wa eneo la ukaguzi wa abiria wanaoondoka ili liweze kuhudumia abiria 300 badala ya abiria 148 waliokuwa wakihudumiwa hapo awali; Miradi inayoendelea ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa kituo cha Mafuta ya ndege (Oilcom); na Mradi wa Ujenzi wa karakana ya matengenezo ya ndege za Kijeshi. 

Aidha, kwa upande wa Miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 ni pamoja na Mradi wa Usimikaji mfumo wa kuratibu miruko/mituo ya ndege na kuhudumia abiria (Common User Terminal Passenger Service - CUTPS), Mradi wa Usimikaji mfumo wa maegesho ya magari na Mradi wa Ujenzi wa uzio wa usalama ambayo iko katika hatua ya uandaaji wa mahitaji.