Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Kiwanja Cha Ndege


Picha za Viwanja Vya Ndege
Taarifa za Viwanja vya Ndege

Kiwanja cha Ndege Bukoba

Historia fupi ya Kiwanja

Kiwanja cha ndege cha Bukoba ni kati ya Viwanja 59 ambavyo vinasimamiwa, kuendeshwa na kuendelezwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kutokana na viwango vya ICAO, Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kipo kwenye daraja la Code 2C  na daraja la tano la Uzimaji Moto na Uokoaji (Fire Category- CAT 5).

Kiwanja hiki kilianzishwa mnamo mwaka 1940 na utawala wa kikoloni baada ya vita kuu ya pili ya Dunia. Baadaye Serikali ya Tanzania ilikikabidhi kwa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania mara baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka kwa lengo la kukisimamia, kukiendesha na kukiendeleza.

Kuanzia mwaka 2008, kiwanja hiki kilifanyiwa maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kurefusha njia ya kutua na kuruka ndege kutoka mita 1200 hadi mita 1500 kwa kiwango cha lami ili kuwezesha ndege aina ya ATR 42 kutua na kuruka kwa usalama.

Maboresho mengine yaliyofanyika ni pamoja na ujenzi wa Jengo jipya la abiria lenye vifaa, mitambo na mifumo mbambali kwa ajili ya kuhudumia abiria na mizigo yao, Jengo la utawala, jengo lenye mfumo/mtambo wa kufua umeme, maegesho ya ndege, barabara ya kuingia/kuondokea ndege.

Kukamilika kwa ujenzi huo kulifanya jengo na miundombinu yake kufunguliwa rasmi na aliyekuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 06/11/2017

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba hupokea ndege na abiria moja kwa moja kutoka na kwenda nchi za nje. Kiwanja kina uwezo wa kuhudumia ndege za ukubwa kama Bombadier Dash 8 -QR 400.

Kiwanja kinatoa huduma za usafiri wa anga kwa masaa 12 kila siku kwa wiki kuanzia mawio na machweo ya jua. Kwasasa barabara za kuondokea, kutua na kuruka ndege hazina taa ili kuruhusu uendeshaji wa ndege ufanyike kwa masaa yote 24 kwa siku 7.

Kiwanja cha ndege cha Bukoba kimepakana na Ziwa Victoria, Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bukoba umbali wa maili 0.5 kutoka Bukoba Mjini/ Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

MIUNDOMBINU YA KIWANJA

Sehemu ya Kuegesha Ndege na Viungio vya Barabara (Apron and Taxiway)

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kina njia moja (Taxiway) ya kuingia/kuondokea ndege na Sehemu ya kuegesha Ndege (Apron) yenye uwezo wa kuegesha ndege 2 za ukubwa wa wastani (Bombardier Dash 8 Q400 na ATR 72) na ndege 2 ndogo aina ya Cessna caravan 208 na hivyo jumla ya ndege 4 huweza kuegeshwa kwa wakati mmoja.

Jengo la Abiria (Interface Infrastructure)

Eneo la Jengo la abiria lina ukubwa wa square meter 1,440 likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka. Jengo hili lina mifumo/miundombinu ifuatayo;

 1. Ukumbi wa abiria wanaoondoka wenye uwezo wa kuchukua abiria 150 kwa wakati mmoja
 2. Ukumbi wa abiria wanaowasili wenye uwezo wa kuchukua abiria Zaidi ya 80 kwa wakati mmoja.
 3. Ukumbi wa watu mashuhuri wenye uwezo wa kuhudumia abiria 10 wakati mmoja.
 4. Madawati 4 ya kukagulia abiria
 5. Mfumo wa kuhudumia mizigo (Baggage Handling System) inayoondoka na inayowasili
 6. Lifti yenye uwezo wa kubeba watu sita
 7. Mfumo wa ufuatiliaji matukio(CCTV Cameras)
 8. Huduma za umeme kutoka TANESCO na Mtambo wa kufua umeme (Stand by generator)
 9. Mfumo wa Kiyoyozi (Cooling system)
 10. Mfumo wa utambuzi moto(Fire detection and alarm system)
 11. Mfumo wa Matangazo (Public Address System)
 12. Mfumo wa kunyonya hewa chafu jengoni( Extract fan system)
 13. Mfumo wa kisasa wa kuchakata maji taka (Modern Sewerage Treatment system).
 14. Miundombinu ya mkongo wa Taifa kwa ajili ya huduma ya WI-FI

Upande wa Nje ya Jengo (Landside Areas)

Upande wa nje ya jengo la abiria kuna huduma na miundombinu ifuatayo:

 1. Eneo la wazi kwa ajili ya abiria wanaosubiri kuondoka, wasindikizaji na wapokeaji
 2. Barabara kwa ajili ya magari kuingia na kutoka kiwanjani
 3. Maegesho ya magari yenye uwezo wa kuchukua magari 95 kwa wakati mmoja
 4. Mgahawa kwa ajili ya abiria, wafanyakazi na wapokeaji/wasindikizaji.

Kiwanja kina huduma za nishati za uhakika za maji, umeme, Simu na Mtandao kwa kutoa huduma bora kwa uendeshaji wa kiwanja. Kiwanja kinategemea umeme kutoka Tanesco na kina mtambo wa kufua umeme wenye ukubwa wa KVA 250. Chanzo kikubwa cha maji ni kutoka BUWASA. Tunapata huduma ya mawasiliano ya simu na mtandao kutoka TTCL kupitia mkongo wa Taifa.

Huduma ya Zimamoto na Uokoaji

Kiwanja kina huduma ya Zimamoto na uokoaji katika daraja la 5 kwa mujibu wa miongozo ya ICAO. Huduma hizo zinajumuisha gari moja la kuzima moto na uokoaji aina ya Benz – STK 2800 yenye uwezo wa kubeba maji lita 5000/foam lita 500 na Dry Chemical powder, 200KG

Udhibiti wa majanga ya ndege hai na Wanyama kiwanjani

Katika kuhakikisha usalama wa kiwanja unakuwepo wakati wote, kiwanja kinaprogramu mahususi ya kukabiliana na majanga ya wanyama na ndege hai wanaoishi kuzunguka eneo la kiwanja.

Takwimu

Mashirika ya ndege yanayotoa huduma

Kiwanja kinatoa huduma kwa ndege zenye ratiba maalumu na zile zisizokuwa na ratiba maalumu (Adhoc). Hivi sasa tuna mashirika ya ndege ya ATCL na Precision Air (ratiba maalum)

Takwimu za miruko ya ndege na abiria

Takwimu za miruko ya ndege, abiria na mizigo kwa Mwaka 2023 ukilinganisha na mwaka 2022 kuanzia mwezi Januari hadi Disemba zinaonyesha kupungua kwa 22.1%, 24.4% kwa idadi ya miruka na mituo ya ndege na abiria na kuongezeka kwa 2.6% kwa idadi ya mizigo na vifurushi.

Mlinganyo wa takwimu kati ya mwaka 2022 na 2023

 

Januari-Desemba 2022

Januari-Desemba 2023

Tofauti

Tofauti (%)

Miruko na mituo ya ndege

1,464

1,141

323

(22.1)

Idadi ya abiria

55,072

41,652

13,420

(24.4)

Mizigo na Vifurushi

20332

20852

520

2.6

MIRADI YA MAENDELEO 

Miradi inayotekelezwa na TAA

Mamlaka ya Viwanja vya ndege inaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kiwanja cha Ndege Bukoba ambayo ni pamoja Mradi wa ujenzi wa Mnara wa kuongozea ndege kiwanjani ambao upo katika hatua za manunuzi ya Mkandalasi wa ujenzi wa mnara huo.