Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Inaunganisha Tanzania na Dunia"
ISO Imethibitishwa 9001:2005; 14001:2015 & 45001:2018

Kiwanja Cha Ndege


Picha za Viwanja Vya Ndege
Taarifa za Viwanja vya Ndege

Kiwanja cha Ndege Bukoba

Historia fupi ya Kiwanja

Kiwanja cha ndege cha Bukoba ni kati ya Viwanja 59 ambavyo vinasimamiwa, kuendeshwa na kuendelezwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kutokana na viwango vya ICAO, Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kipo kwenye daraja la 3C (Code 3c) na daraja la tano la Uzimaji Moto na Uokoaji (Fire Category- CAT 5).

Kiwanja hiki kilianzishwa mnamo mwaka 1940 na utawala wa kikoloni baada ya vita kuu ya pili ya Dunia. Baadaye Serikali ya Tanzania ilikikabidhi kwa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania mara baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka kwa lengo la kukisimamia, kukiendesha na kukiendeleza.

Kuanzia mwaka 2008, kiwanja hiki kilifanyiwa maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kurefusha njia ya kutua na kuruka ndege kutoka mita 1200 hadi mita 1500 kwa kiwango cha lami ili kuwezesha ndege aina ya ATR 42 kutua na kuruka kwa usalama.

Maboresho mengine yaliyofanyika ni pamoja na ujenzi wa Jengo jipya la abiria lenye vifaa, mitambo na mifumo mbambali kwa ajili ya kuhudumia abiria na mizigo yao, Jengo la utawala, jengo lenye mfumo/mtambo wa kufua umeme, maegesho ya ndege, barabara ya kuingia/kuondokea ndege.

Kukamilika kwa ujenzi huo kulifanya jengo na miundombinu yake kufunguliwa rasmi na aliyekuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 15/09/2015.

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kipo katika kundi la daraja la II miongoni mwa viwanja vinne ambavyo vinatoa huduma katika usafiri wa anga (Mwanza, Mtwara, Arusha na Dodoma), pia ni miongoni mwa viwanja ambavyo hupokea ndege na abiria moja kwa moja kutoka na kwenda nchi za nje. Kiwanja kina uwezo wa kuhudumia ndege za ukubwa kama Bombadier Dash 8 -QR 400.

Kiwanja kinatoa huduma za usafiri wa anga kwa masaa 12 kila siku kwa wiki kuanzia mawio na machweo ya jua. Kwasasa barabara za kuondokea, kutua na kuruka ndege hazina taa ili kuruhusu uendeshaji wa ndege ufanyike kwa masaa yote 24 kwa siku 7.

Kiwanja cha ndege cha Bukoba kimepakana na Ziwa Victoria, Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bukoba umbali wa maili 0.5 kutoka Bukoba Mjini/ Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

MIUNDOMBINU YA KIWANJA

Sehemu ya Kuegesha Ndege na Viungio vya Barabara (Apron and Taxiway)

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kina njia moja (Taxiway) ya kuingia/kuondokea ndege na Sehemu ya kuegesha Ndege (Apron) yenye uwezo wa kuegesha ndege 2 za ukubwa wa wastani (Bombardier Dash 8 Q400 na ATR 72) na ndege 2 ndogo aina ya Cessna caravan 208 na hivyo jumla ya ndege 4 huweza kuegeshwa kwa wakati mmoja.

Upande wa Nje ya Jengo (Landside Areas)

Upande wa nje ya jengo la abiria kuna huduma na miundombinu ifuatayo:

  1. Eneo la wazi kwa ajili ya abiria wanaosubiri kuondoka, wasindikizaji na wapokeaji
  2. Barabara kwa ajili ya magari kuingia na kutoka kiwanjani
  3. Maegesho ya magari yenye uwezo wa kuchukua magari 95 kwa wakati mmoja
  4. Mgahawa kwa ajili ya abiria, wafanyakazi na wapokeaji/wasindikizaji.

Kiwanja kina huduma za nishati za uhakika za maji, umeme, Simu na Mtandao kwa kutoa huduma bora kwa uendeshaji wa kiwanja. Kiwanja kinategemea umeme kutoka Tanesco na kina mtambowa kufua umeme wenye ukubwa wa KVA 250. Chanzo kikubwa cha maji ni kutoka BUWASA. Tunapata huduma ya mawasiliano ya simu na mtandao kutoka TTCL kupitia mkongo wa Taifa.

Huduma ya Zimamoto na Uokoaji

Kiwanja kina huduma ya Zimamoto na uokoaji katika daraja la 5 kwa mujibu wa miongozo ya ICAO. Huduma hizo zinajumuisha gari moja la kuzima moto na uokoaji aina ya Benz – STK 2800 yenye uwezo wa kubeba maji lita 5000/foam lita 500 na (Dry Chemical powder, 180KG na 400KGS, Foam Compound, Litres 500 na 2860 Litres.

Udhibiti wa majanga ya ndege hai na Wanyama kiwanjani

Katika kuhakikisha usalama wa kiwanja unakuwepo wakati wote, kiwanja kinaprogramu mahususi ya kukabiliana na majanga ya wanyama na ndege hai wanaoishi kuzunguka eneo la kiwanja.

Takwimu

Mashirika ya ndege yanayotoa huduma

Kiwanja kinatoa huduma kwa ndege zenye ratiba maalumu na zile zisizokuwa na ratiba maalumu (Adhoc). Hivi sasa tuna mashirika ya ndege ya ATCL na Precision Air (ratiba maalum)

Takwimu za miruko ya ndege na abiria

Takwimu za miruko ya ndege, abiria na mizigo kwa Mwaka 2020 ukilinganisha na mwaka 2021 kuanzia mwezi Januari hadi Disemba zinaonyesha kupanda kwa 14%, 21% na 12% 

MIRADI YA MAENDELEO 

Miradi inayotekelezwa na TAA

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kinaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ni pamoja na kupaka rangi jengo la abiria, zimamoto na paa la jengo la utawala, Ununuzi wa vifaa kinga vya Zimamoto na vifaa vya uokozi(vya nchi kavu na majini), ununuzi wa madawa ya kuzimia moto, ununuzi wa magurudumu ya gari la kuzimia moto. 

Uboreshaji wa uzio wa kiwanja kwa mita 700 na uwekaji wa alama za kuongozea ndege(utekelezaji wake kufanyika robo ya mwisho ya mwaka). Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za Ununuzi.

MATARAJIO YA BAADAYE

Serikali ikubali kulitwaa na kuliendeleza eneo la Omukajunguti kwa ajili ya kuwezesha kujenga kiwanja cha ndege kitakachohudumia ndege kubwa zaidi.