DKT POSSI AITAKA TAA KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA ABIRIA MWANZA IFIKAPO DESEMBANaibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Dkt Ally Possi ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Abiria(Terminal Building) katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ifikapo Disemba Mwaka huu ili kurudisha hadhi ya kiwanja hicho  cha ndege kuwa cha Kimataifa.

Hayo ameyasema leo tarehe 18 juni jijini Mwanza alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Jengo la Abiria unaondelea kiwanjani hapo na kuangalia maendeleo ya miradi ya uwekezaji na uendeshaji  inayofanywa na Serikali katika kiwanja cha ndege cha Mwanza ambapo ujenzi wa Kiwanja hicho unarudishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kutoka kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambao ndio wanaosimamia  ujenziwa jengo hilo  kwa sasa.

‘’Natoa Maelekezo kwa TAA kuhakikisha ujenzi wa jengo hili la Abiria unakamilika kufika mwezi Disemba Mwaka huu ili kupunguza Adha ya Usafiri kwa Abiria wanaotumia kiwanja hichi kwa sababu jengo la sasa la Abiria limekuwa dogo na halikidhi mahitaji ya kisasa katika kiwanja chetu’’ alisema Dkt Possi.

Dkt Possi aliongezea kuwa malengo ya Serikali ni kurudisha hadhi ya kiwanja cha  ndege cha Mwanza kuwa cha kimatifa kwa sababu Jiji la Mwanza liko ukanda wa maziwa makuu inayoweza kufanya Mwanza kuwa kituo kizuri cha kuunganisha abiria wanaosafiri kwenda Uganda, Rwanda, Kenya, Burundi na Congo.

Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ni moja ya Viwanja vikubwa nchini na kuna abiria wengi wanotumia kiwanja hiki, pia wafanyabiashara wa Madini na Samaki wanatumia Kiwanja hiki kibiashara sasa lazima kiwanja hiki kiendane na uhalisia wa ukubwa wa Jiji la Mwanza na ndiyo dhamira ya Wizara kuhakikisha Kiwanja hiki kinakuwa cha kimataifa na kutoa fursa kwa watanzania kutumia na kufaidika na kiwanja cha ndege cha Mwanza, Alisisitiza Dkt Possi.

Naye  Mkurugenzi Mkuu TAA Bw Mussa Mbura alisema TAA iko tayari kupokea na kukamilisha ujenzi huo ili kuendana na kasi ya ukuaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza katika kutoa huduma ya Usafiri wa Anga hapa nchini.

"Kiuhalisia hatukuwa na Bajeti ya ujenzi wa jengo hili la Abiria ila haya maelekezo ya Serikali tunayapokea na tutaona namna gani tunapata fedha za kukamilisha huu ujenzi kwa kuomba serikali Kuu kupitia kwa Wizara ili tupate fedha za kumalizia mradi huu na tufungue mipaka kimataifa kutumia uwanja wetu wa Mwanza", Alisema Bw, Mbura.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho Bw, Pascal Kalumbete ameishukuru Serikali kwa kutoa maelekezo ya kukamilika  kwa ujenzi huo kwa sababu kwa sasa Jengo la Abira linalotumika ni la muda mrefu na limezidiwa malengo yake ya kuhudumia abiria laki Mbili kwa Mwaka ambapo kwa sasa jengo hilo linahudumia abiria 350,000  kwa Mwaka.

"Kiukweli Jengo letu ni la muda mrefu sana, Abiria wameongezeka Sana na Miundombinu yake ni ya zamani sana kiasi kwamba hata kufanya Maboresho imekuwa ni gharama sana kwa Mamlaka hivyo kukamilika kwa Jengo hili la Abiria itakuwa chachu kubwa ya Maendeleo kwa Mkoa na Nchi kwa kwa ujumla, Hivyo sisi kama kiwanja tutasimamia na kufanya kazi kwa juhudi ili kufikia malengo ya Serikali katika kiwanja chetu cha Mwanza", alisema Bw Kalumbete.

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu Dkt Possi alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kiwanja cha ndege cha Mwanza ambapo aliagiza Menejimenti ya kiwanja kuhakikisha inasimamia vizuri maswala yote ya usalama katika kiwanja sababu usalama katika kiwanja cha ndege Mwanza umekuwa changamoto ambayo serikali kupitia wizara wanafuatilia kwa ukaribu sana lakini pia kuhakikisha swala la Ndege Hai katika kiwanja cha ndege Mwanza linasimamiwa kwa ukaribu sana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw Mussa Mbura ameitaka Menejimenti ya Kiwanja cha Ndege Mwanza kuwa na mikakati ya kuongeza mapato itakayoenda sambamba na kupunguza matumizi yasiyokuwa na lazima lakini, pia kuhakikisha wanadumisha uadilifu kwa wafanyakazi wote wa kiwanja cha ndege cha  Mwanza na kwa viwanja vingine ikiwa ni pamoja na kutunza siri za Serikali na Abiria na wadau wote wanaohudumiwa viwanjani.


Tanzania Census 2022