Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

WATUMISHI TAA WAPIGWA MSASA JUU YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA KAZI


image title here


Watumishi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuzingatia nidhamu, weledi ,uwajibikaji na utunzaji wa siri wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ili kulinda taswira ya taasisi na Serikali kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja Rasilimali Watu Bw. Wahab Shoo wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanayohusu sheria kanuni na miongozo kuhusu utunzaji wa kumbukumbu, nyaraka na taarifa za Serikali pamoja na kiapo cha utumishi wa umma.

Bw. Shoo amesema mtumishi wa umma anapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu na weledi, kuitumia vema mitandao ya jamii kwa kuandika taarifa sahihi ili kulinda taswira ya Taasisi na Serikali kwa ujumla sanjari na kuzingatia maadili katika utumishi wa umma.

“Ninatoa wito kwa watumishi wate kuyatumia vema mafunzo haya ikiwa ni jitihada za Mamlaka katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji, uadilifu na kuzingatia sheria na kanuni na taratibu za kiutumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kuitumia vema mitandao ya kijamii kwa kuandika habari sahihi zenye kujenga na kulinda maslahi ya taasisi na Serikali kwa ujumla,” amesema Bw. Shoo.


Naye Bi. Pendo Sindato ambaye ni mtoa mafunzo kutoka Ofisi ya Rais, Idara ya Nyaraka na Utunzaji wa Kumbumbuku za Taifa, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Watumishi wa umma juu ya mambo muhimu ya kuyazingatia katika kulinda taarifa na nyaraka za siri za Watumishi na Serikali.

“Utunzaji wa kumbukumbu ni jukumu la kila Mtumishi wa Umma hivyo basi kutokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii na ukuaji wa teknolojia, kumekuwa na tatizo kubwa la uvujaji wa siri , hivyo kupitia mafunzo haya kila mmoja wetu anapaswa kubadilika na kuacha tabia za kutoa siri za ofisi,” amesema Bi. Sindato.

Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia tarehe 13 – 17 Aprili 2026, lengo likiwa ni kuwapa uelewa zaidi Watumishi wa TAA juu ya umuhimu wa utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu sanjari na kuzingatia usiri wa hali ya juu.