Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

Wadau wakutana kujadili utekelezaji wa Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Serengeti


image title here


Wadau wakutana kujadili utekelezaji wa Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Serengeti Wizara ya Uchukuzi na TAA imekutana na wadau wake wakiwemo PSSSF, na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Kampuni ya Saba Engineering ambayo ni Mtaalamu elekezi anayefanya Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti , ili kujadili maendeleo na hatua za utekelezaji wa mradi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambacho kimewaleta pamoja wadau muhimu ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu muelekeo wa mradi huo mkubwa wa kimkakati unaotarajiwa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na utalii nchini.


Akizungumza katika kikao hicho, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Mkurugenzi wa miundombinu Bw. Shomari Shomari amesema anatambua umuhimu wa mradi huo mkubwa na kama Wizara itahakikisha mradi huo unakwenda kwa wakati kama ulivyopangwa.
Kwa upande wa TAA Mkurugenzi Mkuu Bw. Abdul Mombokaleo amesisitiza kuwa mradi huo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa, hususan katika kukuza utalii wa hifadhi ya Serengeti ambayo ni moja ya vivutio vikuu duniani, huku akifafanua kuwa utaongeza uwezo wa kupokea ndege za kimataifa za moja kwa moja na hivyo kurahisisha upatikanaji wa watalii na wawekezaji nchini, na ukiwa umezingatia upatikanaji wa huduma nyingine kama za mahoteli, maduka makubwa n.k tofauti na kuruka na kutua kwa ndege.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo ameeleza dhamira ya taasisi hiyo kushiriki kufadhili mradi huo kikamilifu katika uwekezaji wa miundombinu mikubwa yenye tija kwa taifa, huku akibainisha kuwa mradi huo una matarajio makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo la Serengeti na nchi kwa ujumla.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Serengeti Dkt. Maulid Madeni amesema kwa ushirikiano wa viongozi na wananchi wa Wilaya ya Serengeti wapo tayari ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijamii na mazingira ili kunufaisha wananchi wa maeneo husika.