Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania

"Your Gateway to Global Horizons"
ISO Imethibitishwa 9001:2015; 14001:2015 & 45001:2018

Habari

MOMBOKALEO: TUPIGE KURA KWA WINGI, TUIPELEKE TANZANIA KIMATAIFA ZAIDI


image title here


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo amewaomba watanzania na wadau mbalimbali kupiga kura kwa wingi kukichagua Kiwanja Cha Ndege Cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ili kiweze kushinda tuzo ya ‘World Travel Awards 2026’.

Kupitia tuzo hizo za ‘World Travel Awards’ JNIA imeteuliwa kuwania tuzo kwenye kipengele cha Kiwanja Bora zaidi cha Ndege Afrika kwa mwaka 2026 (Africa’s Leading Airport 2026) huku ikishindana na viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Cape Town, Jomo Kenyata na O.R Tambo.

Akizungumza leo tarehe 27 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa wa Kampeni na zoezi la upigaji kura, Bw. Mombokaleo amewaasa watanzania kupiga kura kwa wingi ili kukichagua Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kushinda tuzo hiyo kwa mwaka 2026 na kuifanya nchi kupaa Kimataifa.
“Sisi hatujaribu, mara nyingi huwa tunatekeleza, nawaomba watanzania wenzangu na marafiki wa Tanzania tupige kura kuichagua Julius Nyerere kwenye tuzo hizi. Hii tunazungumzia Tanzania, na sisi ni wakubwa hatufananishwi na yeyote. Hivyo lazima tupige kura tudhihirishe ukubwa wetu,” amesema Bw. Mombokaleo.

Aidha, Bw. Mombokaleo amesisitiza watanzania kuipigia kura JNIA ili ishinde tuzo hizo na kuiweka Tanzania kwenye ubora Katika sekta ya usafiri wa Anga Kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Bertha Bankwa amewaomba watanzania kupiga kura kwa wingi kuichagua JNIA kushinda tuzo hiyo ya ‘World Travel Awards 2026’. “Hatuna mashaka na kuchukua tuzo hii, hatupati kwa sababu ya kura bali tunaipata kwa sababu tunastahili kushinda tuzo hii,” amesema Bi. Bankwa.

Ikumbukwe Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kiliweza kuchukua tuzo ya ushindi mwaka 2025 kama Kiwanja bora barani Afrika kutoka kwa World Travel Awards.
Kuipigia kura JNIA kama Kiwanja bora barani Afrika Scan Barcode au ingia kwenye link ya Bio iliyopo hapo juu.