Wakwepa kodi marufuku TBIII – Mhe. Naibu Waziri Eng.Nditiye

WAFANYABIASHARA wenye kulipa kodi na kuingizia serikali mapato kwa wakati ndio watakaopata nafasi ya kuwekeza kwenye jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII), imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipofanya ziara ya kutembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kumalizia TBIII.

Mhandisi Nditiye amesema baada ya kukamilika kwa jengo hilo baadaye mwakani, wafanyabiashara watakaopewa kupaumbele hususan waliopo kwenye Jengo la zamani (TBI) na jengo la pili (TBII) ni wale tu wanaozingatia ulipaji wa kodi na mapato yote ya serikali kwa wakati.

"Tunajua wapo wengi waliojitokeza kuomba maeneo ya kufanya biashara, lakini wale ambao watahama kutoka majengo yetu haya mawili la TB I na TBII tunawaambia wazi kabisa kuwa wale waaminifu na waadilifu wenye kulipa kodi ya pango na mapato mengine ya serikali kwa wakati ndio wanafikiriwa kwanza, na wale wasiolipa kwa wakati hawatapewa nafasi kabisa ya kuwekeza kwenye jengo hili," amesisitiza Mhe. Nditiye.

Hata hivyo, Mhe. Nditiye amesema tayari ameuagiza uongozi wa TAA kuhakikisha wanapitia mikataba yote ya biashara kwenye majengo hayo ya abiria na kutengeneza upya ile yenye matatizo ili iweze kuleta tija kwa taifa, kwani kwa sasa kumekuwa na mikataba ya hovyo.

Amesema TBIII inafursa za biashara ambapo inaeneo kubwa la kujenga hoteli, migahawa na sehemu za kupumzikia watu, hivyo kuwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza.

"Juzi tu nilikutana na Wajerumani nikawaeleza tunaeneo la uwekezaji hapa TBIII na kule Msalato mnapotarajia kujenga kiwanja cha kimataifa, na wameonesha nia ya kuja kuwekeza, nia ya serikali na tupo pamoja katika uwekezaji wa maeneo yetu mbalimbali, ili kujiimarisha katika uchumi," amesema Mhandisi Nditiye.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema kuwa wanatarajia watoa huduma na wafanyabiashara watakaokidhi vigezo na masharti ya kutoa huduma bora ndio wakaopata nafasi kwenye jengo hilo la tatu.

"Pia tunatarajia watoa huduma na wafanyabiashara ni wale wanaokodhi vigezo kwa hiyo yote yanalenga katika kuhudumia watanzania na kukuza sekta ya usafiri wa anga na kuhudumia vizuri wale wanaopita hapa," amesema Bw. Mayongela.

Amesema jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria takribani milioni sita (6) kwa mwaka ambalo ni ongezeko kubwa ukilinganisha na jengo la sasa la TBII linauwezo wa kuihudumia kati ya abiria milioni 1.2 hadi 1.5 kwa mwaka.

Hivyo tunaishukuru serikali kwa kutupa ushirikiano katika kuendeleza viwanja vya ndege, pia kwa upande wa TAA wamekuwa wakifanya matengenezo madogo madogo kwa kutumia fedha za bajeti ya ndani.

Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa ameitaka TAA kuwaondoa wafanyabiashara wote wasiolipa kodi na mapato mengine ya serikali kwa wakati, kutokana na kukwamisha juhudi za serikali za ukusanyaji mapato.

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Social Sites & Blog

Feedback & Enquires